Mgomo wa wafanyakazi wa migodi ya dhahabu nchini Afrika Kusini Jumatano
(04.09.2013)umeingia siku yake ya pili wakati hakuna mazungumzo zaidi
yaliyopangwa kufanyika kati ya vyama vya wafanyakazi wa migodi na
waajiri.
Lesiba Seshoka msemaji wa Chama cha Wafanya kazi wa Migodi cha
Taifa(NUM) amesema mgomo huo unaendelea na kwamba hawakualikwa kwa
mazungumzo mapya kujadili madai yao.Chama hicho cha wafanyakazi ambacho
huwakilisha wafanyakazi wote wa migodi wanaogoma kimetupilia mbali
ripoti kwamba imepunguza madai yao ya ongezeko la mishahara kutoka
asilimia 60 hadi kuwa asilimia 10 tu.
Seshoka amesema NUM haikukubali ongezeko la mshahara la asilimia 10 na
kwamba jambo hilo sio kweli,madai yao yako pale pale lakini wako tayari
kwa mazungumzo ya ongezeko la mshahara kupindukia kima hicho.Waajiri
wako tayari kutoaa ongezeko la mshahara la asilimia 6.5.
Maelfu ya wafanyakazi wa migodi ya dhahabu hapo Jumanne (03.09.2013)
walianza mgomo baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya mshahara na kutishia
kusababisha hasara ya mamilioni ya dola kutokana na kukosekana kwa
uzalishaji katika sekta hiyo iliokumbwa na matatizo nchini Afrika
Kusini.
Ulinzi waimarishwa migodini
Hali katika mgodi wa dhahabu wa Doornkop ulioko kilomita 30 magharibi ya Johannesburg hapo Septemba Nne 2013.
Inakadiriwa kwamba wafanyakazi wa
migodi 14,000 wameweka chini nyenzo zao za kazi katika mji wa migodi wa
Carletonville kusini mwa Johannesburg. Usalama kwenye migodi ya eneo
hilo umeimarishwa ambapo walinzi wa kibinafsi wenye silaha wamewekwa
milangoni. Senyen'ge zimezungushwa kwenye lango kuu la mojawapo ya
migodi ya kampuni ya dhahabu ya Anglogold Ashanti.Migodi yote saba
isipokuwa mmoja tu inatarajiwa kuathiriwa na mgomo huo ikiwemo ya
kampuni ya AngloGold Ashanti ,Harmony na Sibanye Gold.
Msemaji wa kike wa sekta ya dhahabu nchini Afrika Kusini Charmane Russel
ameliambia shirika la habari la AFP kwamba sekta hiyo inatazamiwa
kupata hasara ya kilo 761 za uzalishaji wa dhahabu kila siku zenye
thamani ya dola milioni 34.
Mbuyiseli Hiban katibu wa NUM katika mkoa wa mji wa migodi wa
Carlestonville amesema wafanyakazi zaidi wanatazamiwa kujiunga na mgomo
huo leo hii.Amesema huo ni mgomo halali na wafanyakazi hawaogopi
kupoteza ajira zao kama ilivyokuwa huku nyuma
.
Mazingira magumu ya kazi
Mfanyakazi wa mgodi wa kampuni ya dhahabu ya Harmony huko Carletonville kusini mwa Johannesburg.
Wafanyakazi wa migodi hiyo ya dhahabu wanadai ongezeko la
mshahara la kati ya asilimia 60 hadi 100 na kushutumu mishara ya juu
wanayopokea wakurugenzi wakuu wa makampuni ya migodi wakati wafanyakazi
wa migodi wakiishi katika umaskini mkubwa katika nchi hiyo yenye pengo
kubwa kati ya maskini na matajiri.
Mgomo huo utaongeza shinikizo kwa taifa hilo lenye nguvu kubwa za
kiuchumi barani Afrika ambapo takriban wafanyakazi 75,000 katika sekta
ya ujenzi na viwanda vya magari wako katika mgomo.Kwa miongo kadhaa
Afrika Kusini ilikuwa mzalishaji mkuu wa dhahabu duniani lakini fungu
lake la uzalishaji limepungua kutoka asilimia 68 hapo mwaka 1970 hadi
kufikia asilimia sita ya uzalishaji wa jumla wa dhahabu duniani hapo
mwaka jana.
matukio na
IDHAA YA KISWAHILI
/
Matukio ya Afrika