Alhamisi, 17 Oktoba 2013

KARIBU DUNIANI LEO

BURUNDI YAPATA MAKAMU WA RAIS MPYA
 
Busokoza alikuwa mfanyabiashara baada ya kustaafu kutoka katika jeshi

Nchini Burundi, Bwana Bernard Busokoza wa kabila wa watutsi na anayetoka chama cha Uprona, ameteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi .
Bernard Busokoza mwenye umri wa miaka 60 , anachukua nafasi ya Terence Sinunguruza aliyejiuzulu hivi karibuni baada ya kupoteza imani ya chama chake cha Uprona kwa madai kwamba alipuuza maslahi ya chama na kujiendeleza yeye binafsi.
Busokoza alikuwa afisaa wa zamani wa jeshi la zamani la Burundi baada ya kupata elimu ya kijeshi nchini Ugiriki. Hata hivyo alijihusisha na maswala ya biashara hasa katika sekta ya mawasiliano baada ya kustaafu kutoka katika jeshi.
Anamiliki mojawapo ya kampuni kubwa ya mawasiliano nchini humo.
Uteuzi huo wa Bernard Busokoza umeidhinishwa Jumatanojioni na bunge pamoja na baraza la seneti.
Hata hivyo kulikuwa na pingamizi kuhusu uteuzi wake hasa kutoka kwa wabunge wa chama cha (CNDDFDD) cha Rais Pierre Nkurunzinza wakisema kuwa aliwahi kuhusika na mapinduzi ya kijeshi yaliyosababisha kifo cha rais wa kwanza wa kihutu Milkior Ndadai
Makamu wa rais aliyemtangulia, Terence Sinunguruza alijiuzulu kutokana na shinikizo za wanachama wenzake wa (UPRONA) waliodai kuwa haonekani kutetea masilahi ya chama chake.
Chama hicho kilimtaka Rais Pierre Nkurunziza kumfuta kazi Sinunguruza, aliyetuhumiwa kwa kusababisha migawanyiko chamani tangu kuchukua wadhifa huo miaka mitatu iliyopita

WAKIMBIZI WA SYRIA WAENDELEA KUTAABIKA MISRI
Watu wengi nchini Syria wametoroka vita na kukimbilia nchi jirani

Shirika la kimataifa Amnesty International,linasema kuwa maafisa nchini Misri wanawazuilia mamia ya wakimbizi wa Syria katika mazingira mabaya sana.
Wakimbizi hao wanatoroka vita vinavyoendelea Syria.
Katika ripoti yake mpya, shirika hilo linasema kuwa idadi kubwa ya watoto wanazuiliwa wengi wakiwa hawana wazazi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, baadhi ya wakimbizi wamezuiliwa katika vituo vya polisi ambako hali ni duni wengi wakiwa hawapati chakula wala matibabu kwa walio wagonjwa.
Linasema kuwa mjini Alexandria , mapacha wawili wenye mwaka mmoja walipatikana miongoni mwa wale waliozuiliwa.
Maafisa wa utawala bado hawajajibu tuhuma za shirika hilo.
Misri imekuwa ikikumbwa na vurugu za kisiasa tangu kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais Hosni Mubarak mwaka 2011.

WANAJESHI WA UN WAHITAJI VIFAA ZAIDI HUKO MALI
 
NDEGE YA UN NCHINI MALI

Umoja wamataifa umeomba usaidizi wa vifaa kuwawezesha wanajeshi wake wa amani nchini Mali kushika doria.
Kikosi hicho cha UN kilianza kulinda amani nchini Mali mwezi Julai , na kina chini ya nusu ya wanajeshi 12,000 wanaohitajika kushika doria
Mjumbe maalum wa UN nchini Mali, Bert Koenders, amesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni yamekuwa dalili ya changamoto zinazowakumba wanajeshi hao.
Aliongeza kuwa kikosi hicho kinachojulikana kama Minusma, kinahitaji rasilimali zaidi ili kuweze kudhibiti hali Kasakazini mwa nchi.
Wanajeshi wa Ufaransaka , waliongoza operesheni dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu na kuwaondosha kutoka katika eneo hilo.
Uchaguzi wa Urais ulifanyika mwezi Julai lakini wapiganaji hao wakaanza tena kufanya mashambulizi Kaskazini mwa nchi ambako kundi linalotaka kujitawala la Tuareg pamoja na wapiganaji wengine wamekitaka kambi.
Lakini Bert Koenders, anasema kuwa tisho la usalama linasalia kuwa changamoto kubwa.
Mshambuliaji wa kujitoa mhanga alishambulia mji wa Timbuktu tarehe 28 Septemba huku wapiganaji wa kiisilamu nao wakilipiza mashambulizi hayo kwa kurusha makombora.
Kikosi cha kulinda amani cha UN kilipata pigo jengine mwezi Agosti baada ya idadi nyengine kubwa ya wanajeshi wa Nigeria kurejea nyumbani kupambana na wanamgambo wa Boko Haram.
Hatua hii iliwaacha wanajeshi wa UN na chini ya wanajeshi elfu sita. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi wanajeshi 12,640 ifikapo mwezi Disemba.
UN inatarajiwa kuwapeleka wanajeshi wengine huko kuchukua nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa waliorejea nyumbani baada ya kuingilia kati mgogoro huo wapiganaji walipotishia kuvamia mji mkuu wa Mali Bamako mwezi Januari.
Wapiganaji hao wenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeeda walidhibiti Kaskazini mwa Mali, ikiwemo miji mingine mikubwa ya Gao, Kidal na Timbuktu, baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwezi Machi mwaka 2012.

 

Jumatano, 16 Oktoba 2013

USIPITWE NA MATUKIO MBALIMBALI YANAYOTOKEA POPOTE ULIMWENGUNI

WATU WATATU WAZUILIWA KWA MAUAJI HUKO AFRIKA KUSINI
 
 
Mtaa wa Dieplsloot una watu wengi wanaoishi kwa umaskini

Watu watatu wamezuiliwa nchini Afrika Kusini kuhusiana na mauaji ya watoto wawili ambayo yalizua ghasia katika mtaa wa Diepsloot.
Kwa mujibu taarifa ya polisi, miili ya wasichana wawili walio na umri wa miaka miwili na mitatu ilipatikana imetpwa kwenye choo cha umma siku ya Jumanne baada ya wawili hao kupotea siku ya Jumamosi.
Ghasia zilizuka huku wenyeji wakiwatuhumu polisi kwa kukosa kulinda jamii ipasavyo.
Rais Jacob Zuma aliwasihi wasichukue sheria mikononi mwao.
"kitendo hiki cha unyama dhidi ya watoto wetu, sio kitu ambacho kinapaswa kufanywa katika jamii hii ambayo daima tunajitahidi kuiunda,'' alinukuliwa akisema Rais Zuma kwenye jarida moja la mtaani Soweto.
''Tunalaani vikali mauaji haya.''
Luteni kanali Lungelo Dlamini, alisema kuwa watu watatu wanahojiwa na polisi na kuwa wangali wanamsaka mtu wa nne anayeshuiwa kuhusika na kitendo hicho.
Alisema kuwa pia wanachunguza kuwepo uhusiano kati ya mauaji hayo na yale ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano aliyepatikana amefariki katika eneo hilo hilo, mwezi Septemba.
Kulingana na jarida la Star wenyeji wa Diepsloot, jamii masikini Kaskazini kwa Johannesburg, waliweka vizuizi barabarani na kuchoma magurudumu ya magari.
Maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni, yaliporwa huku waandishi wa habari wakishambuliwa.
Wasichana haio walikuwa na uhusiano wa kifamilia , na walipotea Jumamosi nyumbani kwao wakiwa wanacheza na marafiki zao.

MAELFU WATOROKA GHASIA HUKO AFRIKA YA KATI
 
Waasi wa Seleka wanasemekana kuzua rabsha upya katika maeneo ya Magharibi mwa nchi
Shirika la misaada la Medecins Sans Frontieres (MSF), limesema kuwa maelfu ya watu wamelazimika kutoroka makwao katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ghasia zilizoibuka upya.
Nchi hiyo yenye utajiri wa madini, imekuwa ikikumbwa na misukosuko, tangu waasi kumng'oa mamlakani Rais Francois Bozize mnamo mwezi Machi.
Serikali ya Ufaransa wiki hii ilisema kuwa itatuma wanajeshi wa ziada nchini humo katika juhudi zake za kumaliza mgogoro nchini humo.
Wafanyakazi wa afya kutoka katika shirika hilo, wanasema kuwa wanashuhudia visa vya mauaji nchini humo.
Wanawake na watoto ni miongoni mwa watu waliothirika zaidi na ambao wanatibiwa kwa majeraha ya risasi , panga na silaha zengine za kijadi magharibi mwa nchi.
Wafanyakazi wa mashirika ya misaada pia wamekuwa wakishambuliwa.
Vijiji vyote vimeteketezwa na shirika hilo limesema kuwa limepokea visa vya mashambulizi yanayotokana na migawanyiko ya kidini.
Mapigano kati ya makundi ya kutoa ulinzi kwa wanakijiji pamoja na waasi wa zamani yamewalazimisha maelfu kutoroka makwao huku shirika hilo likisema kuwa hali ya kibinadamu sasa ni ya kusikitisha sana na inahitaji kushughulikiwa kwa dharura.

44 WAFARIKI KWA AJALI YA NDEGE LAOS
Uwanja wa ndege Luang

Abiria wote waliokuwa wameabiri ndege nchini Laos wamefariki baada ya ndege iliyokuwa imewabeba kuanguka Kusini mwa nchi.
Maafisa katika nchi jirani ya Thailand wamesema kuwa ndege hiyo ilianguka ndani ya mto Mekong.
Aidha inaarifiwa kuwa ndege hiyo ilianguka kutokana na hali mbaya ya hewa muda mfupi kabla ya kutua katika uwanja wa Pakse.
Ndege hiyo ilikuwa inatoka katika mji mkuu wa Laos wa Vientiane ilipoanguka asubuhi ya leo.
Msemaji katika wizara ya mambo ya nje Sek Wannamethee alisema kuwa abiria 39 na wafanyakazi 4 walikuwa ndani ya ndege hiyo
Alisema rai watano wa Thailand walikuwa miongoni mwa waliofariki.



Jumatatu, 14 Oktoba 2013

VIFO VINGINE NI KAMA VYA KUJITAKIA...ONA YANAYOTOKEA INDIA

109 WAFARUKI KWENYE TAMASHA INDIA
Baadhi ya jamaa za wale waliofariki kutokana na mkanyagano wa watu India 

Idadi ya watu waliofariki katika msongamano wa watu wakati wa tamasha la kihindi, katika mji wa Madhya Pradesh, imepanda na kufika watu 109.
Maafisa wenyeji wanasema kuwa watu wengi walifariki baada ya kutokea mkanyagano karibu na hekalu la Ratangarh viungani mwa mji wa Datia. Wengine walifariki waliporuka kutoka katika daraja hiyo.
Wakati huo huo, miili ya watu hao imechomwa usiku kucha kama ilivyo desturi ya wahindi kwani kwa kawaida hawaziki mtu bali wanachoma mwili wake.

ZIJUE TIMU ZA AFRIKA ZITAKAZOKWENDA KUTIKISA KOMBE LA DUNIA BRAZIL

Nigeria Super Eagles
Nigeria Super Eagles

Ushindi wa Super Eagles ya Nigeria ugenini dhidi ya Ethiopia umeipa matumaini ya kushiriki kombe lijalo la dunia.
Ethiopia ilipata goli la kuongoza kunako dakika ya 56 kupitia mchezaji Asefa.
Bao hilo halikukaa kwa muda mrefu.kunako dakika ya 67 mkwaju uliopigwa na Emanuel Emenike uliishia langoni na kuwa 1-1.
Ethiopia watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi kadhaa walizopata na pengine waliponea chupuchupu kunako dakika 77 ambapo mkwaju wa Nigeria ulirudishwa na mlingoti wa lango.
Goli la ushindi la Nigeria limepatikana kwenye dakika ya mwisho kwa njia ya penalty iliyofungwa kimiani na Emmanuel Emenike na kupalilia njia kwa bingwa hao wa Afrika ya kwenda Brazil.
Didier Drogba
Didier Drogba(kulia)

Ushindi wa Ivory Coast dhidi ya Senegal umekuwa hatua muhimu ya kuelekea katika fainali za kombe la dunia.
Mabao 3 yaliyofungwa na washambuliaji Didier Drogba, Gervinho na Salomon Kalou yametosha kuiongezea matumaini Ivory Coast ya kushiriki fanali za kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil.
Goli la kufutia machozi upande wa Senegal lilifungwa kimiani na mshambuliaji wa NewCastle Papiss Demba Cisse.
Mechi ya mkondo wa pili itachezwa mwezi ujao nchini Morocco kwa sababu Senegal inatumikia adhabu ya kutochezea kwenye uwanja wa nyumbani.

Burkinafaso 3 Algeria 2

Penalti ya dakika za mwisho iliyopewa Burkinafaso katika mazingira ya kutatanisha iliiwezesha timu hiyo kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Algeria.
Hadi dakika ya 85 matokeo yalikuwa magoli 2-2 kabla ya Burkinafaso kupata penalti iliyowawezesha kuondoka na ushindi mdogo.

NI KAULI YA ZITTO KABWE JUU YA MISHAHARA YA WAKUBWA WA NCHI..AANZA NA RAIS,WAZIRI WENGINE WATAFUATA


Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe akizungumza na wananchi.Picha na Maktaba

Zitto alitoa kauli hiyo jana mjini Igunga, wakati akitangaza mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa Zitto, kwa mwaka kiongozi huyo wa nchi analipwa Sh384 milioni ambazo ni wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi. 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe amesema sababu ya kutaja mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo hilo.

Zitto alitoa kauli hiyo jana mjini Igunga, wakati akitangaza mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa Zitto, kwa mwaka kiongozi huyo wa nchi analipwa Sh384 milioni ambazo ni wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi.
Hatua ya Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), kutaja mshahara wa rais inakuja wiki moja baada ya kutaja mshahara wa Waziri mkuu kuwa ni Sh26 milioni kwa mwezi pasipo kukatwa kodi
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi wanancholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho. Alisemaha ni jambo la kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa Sh200,000 kwa mwezi ukikatwa kodi huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi.
Alisema katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara na malipo mengine huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupu rupu kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk Slaa akiwa Rais na akataka kupunguza mshahara wake kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka Serikalini,” alisema Zitto.
Zitto alisema kuwa kitendo cha Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, hakikuzingatiwa kulingana na uwazi uliowekwa kwa kuandika uwazi wa viwango vya mishahara.

Alisema kuwa waziri aliyehusika kufunguia magazeti hayo hakufikiria kwa makini kutokana na kuwa na uelewa mdogo na kuongeza kuwa hakuna kosa lolote linalopelekea kufungiwa magazeti hayo kutokana na ukweli ulioandikwa.