Vurugu hizo zilianza saa 04:42 usiku hadi saa 04:49 usiku wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha Bunge.
Dodoma. Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana usiku kilivunjika baada yavurugu kutawala ukumbini humo.
Vurugu hizo zilianza saa 04:42 usiku hadi saa
04:49 usiku wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha Bunge
hadi leo saa tatu asubuhi.
Chanzo cha vurugu ni kutokana na ugumu wa
kutokukubaliana na azimio la tisa, lililolenga kumwajibisha moja kwa
moja Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Azimio la PAC lilitaka Waziri Muhongo aadhibiwe
kwa kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma zilizokuwa zinazomkabili ikiwamo
kulidanganya Bunge.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wengi wakiwa wa CCM
walitaka waziri huyo asiadhibiwe na Bunge bali achukuliwe hatua na
mamlaka iliyomteua.
Wakati ubishani huo ukiendelea, ikiwa imefika saa
4.42 usiku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
alisimama na Spika Makinda alimruhusu kuzungumza.
“Bunge kufikisha saa tano kasoro ni historia,
lakini leo (jana) kuna uzito wa kiti na uzito wa wabunge kwa mamlaka
ambayo yako ndani yao. Panaonekana kuna maamuzi mengine ya kulinda watu.
Kwa nini leo tuna kigugumizi. Tunapata wakati mgumu kuendelea kushiriki
kikao cha kulindana. Kwanini mnalinda wezi,” ilikuwa ni kauli ya Mbowe.
Mara baada ya kutoa kauli hiyo, wabunge wote wa
upinzani walisimama na kuanza kupiga kelele kwamba wezi
waondoke…tunataka fedha zirudi…tunataka fedha zirudi…vijana
msilale…vijana msilale.