Jumapili, 17 Novemba 2013

JE UNAJUA KUWA NYOKA NA KONOKONO NI TIBA MBADALA KWENYE MWILI WAKO?

 
Nyoka na konokono wamekuwa tiba mbadala kwa watu wengi katika nchi za Ulaya na Asia, ikiwemo kuondoa uzee
Wakati nyoka akiendelea kuwa adui mkubwa wa binadamu na konokono kuonekana mdudu anayetia kinyaa kwa baadhi ya watu, nchi za China na Japan wanyama hawa wamekuwa wakitumika kama mboga na wakati mwingine wamekuwa ni rafiki wa binadamu kwani wengi wao hufugwa na binadamu.
Lakini Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, kwani katika nchi za Ulaya miezi kadhaa iliyopita watu mbalimbali wameanza kupokea tiba kutoka kwa wanyama hao ikiwemo huduma ya kukanda na kupodoa uso (facial) inayotolewa na konokono na kusinga (massage) inayotolewa na nyoka.
Facial ya konokono
Kwa wengi wetu konokono ni mdudu mpole zaidi kuliko wadudu wengine wanaopatikana majanini, lakini nchini Japan wataalamu wamegundua kuwa lami (uteute) anaotoa mdudu huyo ni tiba nzuri kwa ngozi ya binadamu, baada ya kutumika kwa miezi kadhaa nchini Japan sasa tiba hiyo imeanza kupendwa barani Ulaya, kama watu wanavyomiminika katika saluni moja iliyopo East Midland nchini Uingereza.
Matibabu hayo yanahusisha konokono kuanzia watatu ambao huwekwa juu ya uso wa binadamu na wao huanza kuzunguka maeneo mbalimbali ya uso huo, yamekuwa yakiongeza uwingi wa watu katika saluni za maeneo mbalimbali ya nchi za Ulaya.
Wataalamu hao wa facial ya konokono akiwamo Dk Sunil Chopra wanasema kwamba katika matibabu hayo huwa wanahakikisha kwamba konokono anatembelea kila sehemu ya uso wa binadamu isipokuwa maeneo ya mdomo, macho na pua.
Kwa mujibu wa mmiliki wa Simply Divene Saloon iliyopo Corby katika mji wa Northamptonshire nchini Uingereza, Diane Gower matokeo ya tiba hiyo inayogharimu kiasi cha dola 50 sawa na Sh80,000, huonekana papohapo na kwamba wadudu hao hutoa kamasi zenye protini muhimu kwa ngozi ya binadamu.
Anasema, “Mwanzoni kwa mteja wa kwanza huwa wanashtuka sana kwani anapokutembea usoni huona kuwepo kwa hali isiyokuwa ya kawaida, lakini wateja wetu huhisi raha ya ajabu pindi konokono wanapoendelea kutambaa kwenye nyuso zao kwa matibabu.”
Facial ya konokono ilianzishwa katika saluni iitwayo Tokyo’s Clinical Saloon nchini Japan na mtu wa kwanza kupatiwa huduma hiyo alikuwa ni mtu mmoja maarufu nchini humo, Escargot Course mwanzoni mwa msimu huu na kulipia gharama ya dola 161 sawa na Sh 257,600.
Konokono 60 wanamilikiwa na Gower na wamekuwa wakipewa vyakula maalumu, ikiwemo matunda na mboga za majani.
“Hivi sasa watu wengi nchini Japan wanazalisha konokono kwa ajili yetu na hata wengine wanazalisha kwa ajili ya chakula kama utamaduni wetu ulivyo lakini wanatofautiana,” alisema Gower na kuongeza; “Hii si aina ambayo unaweza ukaipata katika bustani, tumekuwa tukiwaelekeza tunahitaji wa aina gani, hata hivyo tunawapa majina ya aina ya konokono tunaowahitaji pia.”
Anasema wafanyakazi wote wa saluni wamepewa mafunzo maalumu ya kushika konokono wanapomhudumia mteja, wengine wanajifunzia katika saluni hiyo na baadaye wanakwenda kufanya kazi sehemu nyingine tofauti.
Hata hivyo kamasi za konokono zinaaminiwa kuwa zina faida kubwa ya kupambana na hali ya kuzeeka.
“Ustawi wa konokono ni muhimu sana kwetu na mara wanapotumika kwa mteja mmoja tunahakikisha hawatumiwi tena angalau kwa kipindi cha siku nne, na tunawaangalia kwa kipindi hicho chote kwani wanakuwa wametoa kamasi kwa wingi mno.”
Gower anasema walihitaji kupata ushauri kutoka kwa watalamu wa konokono namna ya kuwalisha na kuwatunza, ili wasife na namna ya kuweza kuwapa chakula kitakachozalisha kamasi kwa wingi na kusisitiza kwamba wafanyakazi wake wote wameshapatiwa mafunzo hayo.
Baada ya facial
Anasema baada ya kumalizika kwa zoezi la facial konokono hao hutengwa na wengine ili kupata wasaaa wa kuwapumzisha, sambamba na kutoa uchafu wote hivyo kuwepo na usalama wa ngozi za wateja wao.
Hata hivyo, mteja yeyote akishafanyiwa facial hiyo hushauriwa kutotumia kemikali ya aina yoyote kutokana na ulaini wa ngozi zao, hivyo iwapo mteja atakaidi agizo hilo hupata madhara katika ngozi. Gower anasema konokono wana uwezo mkubwa wa kuondoa chunusi ukilinganisha na mafuta mbalimbali yanayotumika kufanya kazi hiyo hata bila kuwa na matokeo kwa uharaka.
“Mara baada ya matibabu haya ya asili ngozi ya uso hubaki katika hali ya uchanga na hupambana na kuzeeka kutokana na kamasi kuwa na mchanganyiko wa viungo vya aside ya ‘hyularonic.” Anasema wanapata wateja wengi ambao hawahitaji kutumia kemikali ili kupambana na kuzeeka kwa ngozi zao.
Dk Chopra ambaye kwa sasa anafanya majaribio ya kliniki juu ya ufanisi wa kamasi za konokono alisema; “Konokono wana kamasi zenye antibiotics na asidi ya hyaluronic ambayo huirudisha ngozi katika uchanga na kuifanya isizeeke kwa urahisi. Tunahitaji kujipanua zaidi katika hili. Wenzetu Ufaransa wamegundua kwa kuchukua kamasi za konokono na kuzihifadhi kama bidhaa ya huduma ya facial, lakini sisi tunatumia konokono halisi.”
Kusinga ‘massage’ ya nyoka
Nchini Tanzania wapenzi wa kusingwa maarufu kama ‘massage’ wamezoea kufanyiwa huduma hiyo na binadamu wenye mikono laini, lakini hali ni tofauti huko nchini Indonesia ambapo hivi sasa huduma hiyo imekuwa ikitolewa na nyoka.
Hata hivyo bado wateja si wengi kutokana na woga wa kung’atwa na nyoka hao. Katika moja ya ofisi zinazotoa huduma hiyo katika Mji wa Jakarta nchini Indonesia, Feri Tilukay ni mmoja wa wateja ambaye kutokana na woga amefumba macho huku akiendelea kupata huduma hiyo kutoka kwa nyoka watatu aina ya ‘enormous’.
Akizungumza na Shirika la Habari la AFP, Tilukay mwenye umri wa miaka 31 anasema; “Nimejisikia vizuri sana yaani anatembea huku akikakamaza mwili wangu ni kusinga kwa ajabu kwa kweli.”
Nyoka hao wana majina maalumu, kuna Jasmine, Muscle na Brown ambao hufanya kazi ya kwanza ambayo itamlazimu mteja kulala chali na wao kupita juu ya mwili wale. Baadaye hutembea mpaka shingoni na kusinga kwa muda kisha hushuka mpaka kiunoni.
Kabla ya kuanza kazi nyoka hao hufungwa kwa mikanda maalumu mdomoni mwao, ili kuhakikisha hawawezi kumdhuru mteja na hubandikwa plasta maalumu ili kutotoa hata tone la sumu ambayo inaweza kudhuru ngozi ya mteja.
Matibabu hayo ya dakika 90 hugharimu rupia 480,000 sawa na dola 43 ambapo kwa fedha za Tanzania ni Sh 69,000.
Nchini Indonesia kuna wateja wachache ambapo walio wengi hutokea bara la Ulaya, Japan au Korea Kusini kwa mujibu wa meneja wa kituo hicho, Paulus Abraham.
Ingawa watu wengi wanaopata singa katika kituo hicho cha Bali Heritage Reflexology ni mahiri na wasio na waoga, kituo hicho kipo katika matangazo ya kuhamasisha watu kusinga hiyo kwani ina manufaa kwao.
“Nilikuwa na hofu ya nyoka yaani nilikuwa mwoga sana kwa wanyama hawa lakini baada ya kupata matibabu mara kadhaa nimekuwa vizuri,” alisema Tilukay ambaye amesingwa na nyoka kwa zaidi ya mara tatu.
Singa ya nyoka ni moja kati ya matibabu zaidi ya 300 yanayotolewa katika kituo hicho. Huduma hii ilianza kutolewa katika kituo hicho mwaka mmoja uliopita na imekuwa ikiwavutia wengi.
Nyoka hao wanatunzwa katika nyumba moja iliyojengwa kwa kutumia mbao katika kisiwa kimoja kilichopo Bali, na wamekuwa wakilishwa chakula cha sungura ili kuishi.
Hata hivyo haki za wanyama pamoja na watu wa haki za binadamu wamekuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na tiba hiyo. Watu wa haki za wanyama wameizungumzia tiba hiyo kama ‘unyonyaji’.
“Tunachukizwa kusikia kuhusu aina yoyote ya unyonyaji dhidi ya wanyama wakiwamo nyoka,” alisema mmoja wa wanaharakati hao wa haki za wanyama Benvika.
Hata hivyo, meneja wa kituo hicho Abraham alisema; “Sisi hatuwachukui kutibu watu kama wafanyakazi, tunawachukulia kama marafiki zetu au familia,” alisema na kuongeza; “Tunawabusu, tunawakumbatia na tunawapa huduma nzuri sana.”
 
 

Hakuna maoni: