Maelfu ya wakimbizi ambao wamekuwa wakitoroka nchi ya Sudan Kusini
kutokana na vita nchini humo wamehamia Uganda. Mpigaji Picha, Fredric
Noy, anayefaifanyia kazi Idara ya wakimbizi ya Umoja wa mataifa,
anatumia picha, kufarisia maisha ya ukimbizi ya Atem Angang na familia
yake.
Mji wa Bor alimokuwa anaishi Matiop Atem Angang ndilo lililokuwa la
kwanza kudhibitiwa na waasi pindi vita vilipozuka Sudan Kusini mnamo
Desemba 15. Yeye pamoja na familia yake kubwa ya watu 15, akiwemo mamake
wa miaka 95, watoto wake sita pamoja na familia ya dadake walitoroka
kutoka nchini humo.
Bor, mji mkuu wa Jimbo la Jonglei, umekuwa chini ya udhibiti ambao
umekuwa ukibadilika kati ya waasi, na serikali mara kwa mara, na
imewaacha watu wengi wakiwa wamepoteza maisha. Tangu makubaliano ya
kusitisha mapigano kuafikiwa Januari, pande hizo mbili zimekuwa
zikilaumiana. Familia ya Bw. Angang imesafiri kwa muda wa wiki moja kwa
kutumia dau na lori ili kufika Uganda.
Mpakani, walipelekwa kwa kituo cha Shirika la Umoja wa Kimataifa
linalotetea haki za kibinaadam lililoko Adjumani, kaskazini mwa nchi
hiyo. Wananchi wengi wa Sudan Kusini wanatoroka nchi hiyo, na hii
imekifanya kituo hicho kujaa wakimbizi wapya kila uchao. Umoja wa
mataifa unasema kuwa takriban watu 860,000 wametoroka kutoka Sudan
Kusini tangu kuibuka kwa vita nchini humo.
Lori linalowasafirisha wakimbizi kutoka Sudan, akiwemo Bw. Angang na
familia yake, linavuka daraja kabla ya kufika kituo cha uhamiaji cha
Dzaipi. Lori hizo husafiri hadi mara nne kwa siku kati ya mipakani na
kituo hicho cha uhamiaji.
Maafisa wa Uganda wanajaribu kuondoa vifaa vya vita kutoka makao hayo, huku wakipekua vitu walivyonavyo wakimbizi wanaofika.
Mamake Angang’, Apiou Angar, ambaye ni mkongwe, anakutana na rafiki yake
wa zamani wakiwa safarini. Bor, mji ambao ulikuwa unajivunia idadi ya
watu 25,000, sasa umebaki mtupu.
"Hii familia ina bahati sana ikilinganishwa na zile ambazo itabidi
zingoje kwa majuma mawili ili ziweze kuhama na kuenda kuanza maisha
mapya katika makao mageni,” hii ni kulingana na Shirika la kutetea haki
za kibinaadam la Umoja wa mataifa. Bw. Angang amepiga hema (kulia)
kutumia vifaa alivyobeba kutoka Bor.
Famililia hii haijazoea makali ya baridi nyakati za usiku, ila
walivumilia. Asubuhi ilipofika, akisaidiwa na mkalimani, Bw. Angang
aliweza kuisajili familia yake na Shirika la msalaba mwekundu la Uganda.
Baada ya kulala chini ya hema ambayo haiwezi kuwakinga kutokana na
makali ya baridi kwa siku mbili, watoto wake wanakuwa wagonjwa. Katika
kituo cha afya kilichoko karibu, wahudumu wa afya nchini humo wamekuwa
wakiwahudumia wagonjwa kwa masaa 12 kutokana na uongezekaji wa idadi ya
wakimbizi
Mpwa wa Bw. Angang ambaye ana miezi sita, Nyalet Deng, anachunguzwa na
daktari wa kiliniki inayopata ufadhili kutoka kwa shirika la Medicines
Sans Frontieres (MSF) iwapo anaugua utapiamlo.
Baada ya siku tatu katika kituo cha uhamiaji, familia hiyo inawasili
katika makao ya Nyumanzi-mahala ambapo watapaita nyumbani pindi
watakavyoendelea kuishi Uganda.
Wakati ambapo Bw. Angang na familia yake inangoja kando ya barabara
kupewa kipande cha ardhi, wanapiga hema itakayowasaidia kujikinga dhidi
ya makali ya jua la mchana.
Bw. Angang anaugua malaria, na sasa itambidi bintiye wa miaka 18 kuendea
chakula cha mwezi cha familia hiyo kutoka kwa Shirika la chakula
duniani. Familia nzima ya Bw. Angang inangoja kwa matumaini iwapo
majadialiano ya kusitisha vita nchini Sudan Kusini kati ya serikali na
waasi mjini Addis Ababa, Ethiopia,yatavuna matunda.