AU KUJADILI UHUSIANO WAKE NA ICC
AU inajadili swala hili baada ya ICC kupuuza ombi la kutaka kuhamisha kesi za Kenyatta na Ruto
Marais wa Afrika wanakutana
wikendi hii mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili uhusiano wa bara
la Afrika na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.
Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC
kukataa ombi la wanachama 54 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za
Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani.
Viongozi hao wanatarajiwa kujadili hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya
ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU katika
kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na
mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa
kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za
Kenya. AU inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa
kiafrika.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake
William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu
katika mahakama hiyo.
Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.
Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.
Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya
wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya
kuondoa Kenya kutoka katika mahakama ya ICC.
Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza
nchi za Afrika kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na
majirani zake kama Uganda na Rwanda.
Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.
Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU
isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na
Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa ICC.
WABAKAJI WAADHIBIWA KWA KUKATA NYASI KENYA
Mwathiriwa alisema kuwa anawajua wabakaji
Wakenya wameghadhabishwa sana na
hatua ya wanaume watatu waliombaka msichana mmoja na kutupa mwili wake
kwenye choo kuamrishwa na polisi kukata nyasi kama adhabu kwao.
Msichana huyo alishambuliwa na kubakwa akiwa njiani kutoka kwa mazishi ya babu yake katika kijiji kimoja Magharibi mwa nchi.
Kwa mujibu wa taarifa za gazeti la Daily Nation
nchini Kenya, uti wa mgongo wa msichana huyo ulivunjika wakati wa
ubakaji na sasa amelazimika kutumia kiti cha magurudumu.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na wabunge wamelaani polisi kwa kukosa kuchunguza madai ya msichana huyo.
Msichana huyo alinukuliwa akisema kuwa anataka waliomfanyia kitendo hicho kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Idara ya polisi inawachunguza polisi waliopokea
malalamishi ya msichana huyo , alisema Halima Mohammed , kamanda wa
polisi katika jimbo la Busia ambako kitendo hicho kilitokea.
Hii bila shaka inaonyesha wazi ulegevu wa polisi
katika kukabiliana na vitendo kama hivi na ambao wakenya wanahisi kuwa
unakumba idara ya polisi , hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi nchini
humo wiki mbili zilizopita.
Msichana huyo aliwafahamu vyema waliombaka na polisi walirekodi kesi dhidi ya watatu hao.
Wanakijiji waliwapeleka watatu hao kwa polisi baada ya kusikia taarifa za kitendo hicho.
Lakini waliamrishwa kukata nyasi katika bustani la makao ya polisi na kisha baadaye kuachiliwa, alisema mamake mwathiriwa.
Masaibu ya msichana huyo yalijadiliwa na kamati
ya bunge kuhusu usalama na kusema kuwa kitendo hicho ni cha kushutua
sana na lazima wakifanyie uchunguzi.
Kwa mujibu wa Bi Mohammed, mama ya msichana huyo
aliamrishwa kumsafisha mwanawe ili ushahidi wowote dhidi ya washukiwa
uweze kupotea.
Msichana huyo sasa amelemazwa na kulazimishwa kutumia kiti cha mgurudumu.