Ijumaa, 20 Desemba 2013

UGANDA....MASHOGA, WASAGAJI KUFUNGWA MAISHA

 
Muingereza David Cicil gerezani kwa madai ya tamthilia chafu
Uganda imepitisha mswada unaopinga mapenzi ya jinsia moja.
Iwapo Rais Yoweri Museveni ataidhinisha sheria hiyo inamaanisha atakayepatkana na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Mswaada huo uliopitishwa na bunge siku ya Ijumaa halikadhalika inasema mtu yeyote aliye na taarifa za watu wanoshiriki mapenzi ya jinsia moja na kushindwa kuripoti habari hizo kwa maafisa wa polisi atafungwa gerezeni maisha.
Wakati hu huo bunge hilo hilo la Uganda siku ya Alhamisi liliidhinisha mswaada unaopiga marufuku maonyesho ya picha za chafu.
Mswada huo unaharamisha kitu chochote kitakachoonyesha sehemu nyeti kama vile matiti, mapaja, makalio au tabia yoyote inayozua uchu wa mapenzi.
Kulingana na mswada huo, sheria iliyopo sasa kuhusu picha chafu haihusu zaidi picha hizo bali linahusu uchapishaji ,mawasiliano, taarifa , burudani, maonyesho katika kumbi za kuigizia, miziki inyochezwa katika vyombo vya habari, densi, sanaa, mitindo na picha za runinga.
Mapema mwaka huu Waziri wa maadili wa Uganda, Simon Lokodo, alipendekeza kuwa mwanamke yeyote anayevalia nguo ambayo inafika juu ya magoti anatakiwa kukamtwa na kuadhibiwa kisheria.
Mswada huo unahitaji kuidhinishwa na Rais kabla ya kufanywa sheria.
Uganda ni nchi inayoshikilia mawazo ya kihafidhina yaani isiyopendelea mageuzi katika mawazo na inaandaa sheria ya kuwaadhibu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja ikijumuisha hukumu ya kifo katika baadhi ya kesi.

WAASI WAENDELEA KUUA WATU AFRIKA YA KATI....1000 WAPOTEZA MAISHA

 
Wanamgambo wa kundi la anti-balaka, Jamhuri ya Afrika ya Kati
Takriban watu elfu moja wameuawa na waasi wa zamani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mapambano yaliyodumu kwa siku mbili yaliyojitokeza mwezi huu, makadirio haya yanazidi yale ya Umoja wa Mataifa. Shirika la Amnesty International limesema.
Shirika hilo limesema kuwa uhalifu wa kivita bado unaendelea kufanyika nchini humo.
Wapiganaji hao ambao wengi wao ni Waislamu walimuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, Francois Bozize mwezi March, hali iliyosababisha mgogoro ndani ya jamii nchini humo.
Kiongozi wa waasi Michel Djotodia hivi sasa ni kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Waislamu anayeongoza taifa lenye Wakristo wengi na ndiye kiongozi wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati.
Katika ripoti hiyo, Amnesty International imesema waasi wa zamani wa Seleka waliwaua takriban watu 1000 mjini Bangui, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kulipa kisasi dhidi ya wapiganaji wa Kikristo wanaodaiwa kuwashambulia waasi wa Kiislam.
Idadi ya waliopoteza maisha imeelezwa kuongezeka kuliko ile iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ambao ulisema watu 450 waliuawa mjini Bangui na wengine 150 sehemu nyingine nchini humo.
Mashambulio hayo yamekuja baada ya wanamgambo wajulikanao kwa jina la anti-balaka ambao walikuwa wakiingia kila nyumba na kuwaua watu 60 wa jamii ya Kiislamu. Amnesty International imeeleza.

Askari wa Ufaransa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Mashambulio yaliyofanywa na wanamgambo wa zamani wa Seleka yamehusisha mauaji pia uvamizi na uporaji katika nyumba za raia,ambapo wanawake na watoto kadhaa wameuawa.
Shirika hilo limesema kuwa raia huuawa kila siku mjini Bangui, ingawa kumekuwepo na vikosi vya Ufaransa na Umoja wa Afrika, Ufaransa ikiwa na askari 1,600 nchini humo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wapiganaji wa Kikristo walishambulia jamii ya kiislamu kaskazini mwa mji wa Bossangoa na kuwachinja watoto huku wakiwashinikiza wazazi wao kushuhudia mauaji hayo.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Djotodia aliiambia redio ya Kifaransa kuwa yuko tayari kuzungumza na viongozi wa wanamgambo wa Kikristo ili kutatua mzozo huo.
Kauli hiyo imekuja baada ya Umoja wa Afrika kuidhinisha kuongeza vikosi vyake na kufikia askari 6,000.
Vikosi vya Umoja wa Afrika na vya Ufaransa vinafanya jitihada za kuwanyang'anya silaha wanamgambo hao.