Jumatano, 4 Septemba 2013

Rais mpya wa Mali aapishwa

Rais mpya wa Mali Ibrahim Boubacar Keita

Rais mpya wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, ameapishwa kama rais wa nchi hiyo mjini Bamako.
Sherehe kubwa zaidi ambapo rais wa Ufaransa Francois Hollande amealikwa zitafanyika baadaye mwezi huu.

Wanajeshi wa Ufaransa walisaidia jeshi la Mali kupambana na wapiganaji wa kiisilamu waliokuwa wameteka eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo mapema mwaka huu.

Mtangulizi wa Keita ambaye kwa sasa ni kaimu rais, Dioncounda Traore, alisema mnamo Jumatatu kuwa tayari amekabiliana na changamoto kubwa sana ikiwemo kuandaa uchaguzi wa amani na kuweza kudhibiti maeneo yaliyokuwa yametekwa na waasi.

Duru zinasema kuwa bwana Keita atastahili kukabiliana na maswala muhimu zaidi kama vile kuleta uthabiti katika eneo la Kaskazini na kuleta mageuzi katika jeshi pamoja na kupambana na ufisadi.

Jose Mourinho amfananisha Mesut Ozil na akina Figo na Zidane

Ten out of ten: Jose's a big fan of Arsenal's new boy Mesut Ozil
Bosi wa Chelsea Jose Mourinho

Asema Ozil kusaini mkataba na Arsenal ataifanya Club hiyo kuwa hadhi kubwa Duniani, na ndiyo maana waliamua kutomuuza Demba Ba kwenda katika Club hiyo yenye makazi yake katika jiji la London.

"Ozil ni mtu wa kuigwa na mtu yeyote, yeye ni namba kumi bora duniani .Amefanya mambo kuwa mepesi kwangu na kwa timu yake pia kwa maamuzi aliyo yafanya"

"Kila mtu anampenda..vitu walivyofanya akina Luis Figo na Zinedine Zidane vinaonekana kwake" alisema Bosi huyo wa the Blus

Morinho amesema kumuuza Ozil kwa Club hiyo ya Arsenal kumemfanya ashindwe kuwapa Demba Ba kwa mkopo hivyo ndiyo maana kumeongezeka kwa upinzani mkupwa kwenye Ligi.


Wafanyakazi wa migodi ya dhahabu wagoma

Mgomo wa wafanyakazi wa migodi ya dhahabu nchini Afrika Kusini Jumatano (04.09.2013)umeingia siku yake ya pili wakati hakuna mazungumzo zaidi yaliyopangwa kufanyika kati ya vyama vya wafanyakazi wa migodi na waajiri. 

Lesiba Seshoka msemaji wa Chama cha Wafanya kazi wa Migodi cha Taifa(NUM) amesema mgomo huo unaendelea na kwamba hawakualikwa kwa mazungumzo mapya kujadili madai yao.Chama hicho cha wafanyakazi ambacho huwakilisha wafanyakazi wote wa migodi wanaogoma kimetupilia mbali ripoti kwamba imepunguza madai yao ya ongezeko la mishahara kutoka asilimia 60 hadi kuwa asilimia 10 tu.

Seshoka amesema NUM haikukubali ongezeko la mshahara la asilimia 10 na kwamba jambo hilo sio kweli,madai yao yako pale pale lakini wako tayari kwa mazungumzo ya ongezeko la mshahara kupindukia kima hicho.Waajiri wako tayari kutoaa ongezeko la mshahara la asilimia 6.5.

Maelfu ya wafanyakazi wa migodi ya dhahabu hapo Jumanne (03.09.2013) walianza mgomo baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya mshahara na kutishia kusababisha hasara ya mamilioni ya dola kutokana na kukosekana kwa uzalishaji katika sekta hiyo iliokumbwa na matatizo nchini Afrika Kusini.

Ulinzi waimarishwa migodini
Hali katika mgodi wa dhahabu wa Doornkop ulioko kilomita 30 magharibi ya Johannesburg hapo Septemba Nne 2013.  
Hali katika mgodi wa dhahabu wa Doornkop ulioko kilomita 30 magharibi ya Johannesburg hapo Septemba Nne 2013.
 
Inakadiriwa kwamba wafanyakazi wa migodi 14,000 wameweka chini nyenzo zao za kazi katika mji wa migodi wa Carletonville kusini mwa Johannesburg. Usalama kwenye migodi ya eneo hilo umeimarishwa ambapo walinzi wa kibinafsi wenye silaha wamewekwa milangoni. Senyen'ge zimezungushwa kwenye lango kuu la mojawapo ya migodi ya kampuni ya dhahabu ya Anglogold Ashanti.Migodi yote saba isipokuwa mmoja tu inatarajiwa kuathiriwa na mgomo huo ikiwemo ya kampuni ya AngloGold Ashanti ,Harmony na Sibanye Gold.

Msemaji wa kike wa sekta ya dhahabu nchini Afrika Kusini Charmane Russel ameliambia shirika la habari la AFP kwamba sekta hiyo inatazamiwa kupata hasara ya kilo 761 za uzalishaji wa dhahabu kila siku zenye thamani ya dola milioni 34.

Mbuyiseli Hiban katibu wa NUM katika mkoa wa mji wa migodi wa Carlestonville amesema wafanyakazi zaidi wanatazamiwa kujiunga na mgomo huo leo hii.Amesema huo ni mgomo halali na wafanyakazi hawaogopi kupoteza ajira zao kama ilivyokuwa huku nyuma
.
Mazingira magumu ya kazi
Mfanyakazi wa mgodi wa kampuni ya dhahabu ya Harmony huko Carletonville kusini mwa Johannesburg.  
Mfanyakazi wa mgodi wa kampuni ya dhahabu ya Harmony huko Carletonville kusini mwa Johannesburg.
Wafanyakazi wa migodi hiyo ya dhahabu wanadai ongezeko la mshahara la kati ya asilimia 60 hadi 100 na kushutumu mishara ya juu wanayopokea wakurugenzi wakuu wa makampuni ya migodi wakati wafanyakazi wa migodi wakiishi katika umaskini mkubwa katika nchi hiyo yenye pengo kubwa kati ya maskini na matajiri.
Mgomo huo utaongeza shinikizo kwa taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika ambapo takriban wafanyakazi 75,000 katika sekta ya ujenzi na viwanda vya magari wako katika mgomo.Kwa miongo kadhaa Afrika Kusini ilikuwa mzalishaji mkuu wa dhahabu duniani lakini fungu lake la uzalishaji limepungua kutoka asilimia 68 hapo mwaka 1970 hadi kufikia asilimia sita ya uzalishaji wa jumla wa dhahabu duniani hapo mwaka jana.

matukio na IDHAA YA KISWAHILI / Matukio ya Afrika

Muandaaji pambano la Cheka kutinga kortini


Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Suleiman Kova
Muandaaji wa pambano la kimataifa la ngumi kati ya bondia Francis Cheka wa Tanzania na Mmarekani Phil Williams, Jay Msangi yuko katika hatari ya kuburuzwa mahakamani wakati wowote kuanzia leo kutokana na tuhuma za kumdanganya Mmarekani huyo na kutomlipa fedha walizokubaliana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kwamba muandaaji huyo bado anashikiliwa na polisi na kwamba, ikibainika ni kweli amedanganya na kutolipa fedha hizo kama walizokubaliana atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani.

Akieleza zaidi, Kova alisema kuwa kwa kawaida huwa kuna mambo matatu yanayofanywa kabla ya pambano lote la ngumi na mojawapo ni makubaliano juu ya malipo.
 
"Mabondia kabla ya kupigana lazima wafanye mambo matatu... lazima waongee na mawakala wao, lazima wasaini mikataba kuhusiana na maslahi na pia wakubaliane kuwa watapigana kwa raundi ngapi," alisema Kova, akiongeza kuwa mwandaaji huyo bado anashikiliwa na polisi katika kituo cha Kati jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.

"Tunatakiwa kuwa wakali hata katika michezo kwavile mapambano ya aina hii yanayotajwa kuwa ni ya kimataifa huitangaza nchi hadi nje ya mipaka yetu... sisi (polisi) tunaendelea na uchunguzi wetu ili kubaini kilichotokea," alisema Kova.

Taarifa zaidi zilieleza baadaye jana kuwa muandaaji huyo anadaiwa na Mmarekani Williams dola za Marekani 8,200 (Sh. milioni 13).

Katika pambano hilo la raundi 12 kuwania mkanda wa WBF, uzani wa 'super middle' lililofanyika Ijumaa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Cheka alitwaa ubingwa huo baada ya kushinda kwa pointi.

Dalili za utata wa malipo katika pambano hilo zilianza kuonekana mapema baada ya mabondia Alfonce Mchumiatumbo aliyepigana na Chupac Chipindi katika pambano lao la utangulizi la raundi sita kugoma kupanda ulingoni hadi wamaliziwe pesa zao za mkataba wa kucheza mechi hizo kabla ya kupanda ulingoni, sawa na kile walichokifanya mabondia Mada Maugo na Thomas Mashali ambao pia walikataa kupanda ulingoni hadi walipohakikishiwa kulipwa fedha zao.

Putin aonya Marekani kuhusu Syria

                                              Rais Vladmir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin, ameonya Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya kushambulia Syria.

Alisema kuwa hatua zozote za kijeshi dhidi ya Syria itakuwa ni uvamizi.
Rais wa Marekani Barack Obama ametoa wito wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria baada ya kusema kuwa kuna thibitisho kuwa rais Assad ametumia silaha za kemikali dhidi ya wananchi wake.

Lakini kwenye mahojiano na shirika la habari la Associated Press, kabla ya mkutano wa wiki hii wa G-Twenty mjini St Petersburg, bwana Putin alisema kuwa huenda akaunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa ikiwa kuna thibitisho kuwa silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya raia.

Putin pia alipuuza wasiwasi kuwa wanariadha au mashabiki wataadhibiwa ikiwa watatoa matamshi yatakayoonekana kuwa propaganda kuhusu mapenzi ya jinsia moja wakati wa michezo ya olimpiki itakayofanyika nchini humo.

Wakati huohuo , maseneta nchini Marekani wameridhia mswada wa azimio linalompa idhini Rais Barack Obama kutekeleza shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Mswada huo utapigiwa kura wiki ijayo.
Awali Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alifika mbele ya Baraza la Senate ambapo alitoa onyo kwa maseneta wa Marekani kabla ya mdahalo wao kuhusu Syria unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo kwamba, hawapaswi kushindwa kutoa jibu la kile alichokitaja kuwa ni matumizi ya silaha za kemikali ambayo hayawezi kukanushwa yaliyofanywa na Rais Assad kwa watu wake mwenyewe .

Naye Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuwa ikiwa itathibitishwa kwamba silaha za sumu ya kemikali zilitumiwa nchini Syria , baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lazima liungane na kuchukua hatua.

Wabunge Z’bar wakwamisha Muswada wa kura za Maoni


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huviza akijibu swali bungeni Dodoma jana.

Dodoma. Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 uliokuwa ujadiliwe katika mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umeondolewa na sasa utajadiliwa Bunge lijalo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema kwamba kuahirishwa huko kumetokana na wajumbe wa

Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.
Muswada huo ulikuwa ujadiliwe na wabunge katika kikao cha Bunge kinachoendelea ukitanguliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.

“Ukisoma huu Muswada unasema kura hiyo itapigwa Tanzania Bara na Zanzibar sasa sheria hii ina apply vipi (inatumikaje) Zanzibar wakati kule tuna sheria yetu tayari?” alihoji Mbunge mmoja wa Zanzibar.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa jana, alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo wa kura ya maoni kusema na utakaojadiliwa ni ule wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee.

“Bunge litaahirishwa Ijumaa (keshokutwa) na ni kweli huo Muswada wa Kura ya Maoni umeondolewa kwa sababu bado uko kwenye ngazi ya kamati,” alisema Joel.
Alipoulizwa sababu za kuondolewa kwa muswada ambao ulishaingizwa kwenye ratiba ya Bunge, alitaka swali hilo aulizwe Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Waziri Lukuvi alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo na kusema utajadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Oktoba.

“Ni kweli muswada huu hautajadiliwa na Bunge hili bado kuna mashauriano yanaendelea kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema wabunge wa Zanzibar ndiyo waliokwamisha muswada huo kutokana na mgongano wa sheria.

“Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni mgongano,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema tangu mwanzo aliliona suala hilo na kuitahadharisha Kamati ya Bunge kwamba mapendekezo hayo yana upungufu.

Muswada pekee uliobaki wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unatarajiwa kuwasilishwa leo huku ukitarajiwa kuibua mjadala mzito kutokana na misimamo ya baadhi ya wabunge.
Muswada huo unawasilishwa wakati CCM kikiwa kimeweka msimamo wa kupinga baadhi ya mambo katika Rasimu ya Katiba.
 
 
Yanayotarajiwa kuzua mjadala
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amekiri kupokea mapendekezo kutoka kwa wabunge na hasa kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba akisema wametaka kuangaliwa upya kwa kipengele cha Kamati ya Uteuzi ya viongozi wa Bunge la Katiba. Alisema sasa wataweka sifa za mwombaji wa nafasi hizo na wasiokuwa nazo hawatagombea.
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unataka wawakilishi kutoka makundi ya jamii kuwa 166 katika Bunge la Katiba, lakini wabunge wanataka idadi iwe 200.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema uzoefu katika nchi nyingine unaonyesha kuwa mabunge ya Katiba hushirikisha watu wengi ili kupata uwakilishi mpana tofauti na mapendekezo yaliyotolewa.

Mkosamali ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema ni vyema sheria ikasema wajumbe wa Bunge hilo watatoka katika taasisi zipi.

Kifungu kingine ni kile kinachohusu Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu wake ambao kwa mujibu wa muswada itaundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG) na yule wa SMZ, Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Bara na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar na Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mkosamali alisema muswada huo wa Mabadiliko ya Katiba unasema mwenyekiti wa muda atakuwa Spika wa Bunge lakini akataka: “Mwenyekiti wa muda atokane na Chama cha Majaji wastaafu maana wao hawafungamani na upande wowote.”

Wachimba migodi waanza mgomo A.Kusini

Mgomo huu unatishia kuathiri sekta ya madini nchini Afrika Kusini

Takriban wachimba migodi 80,000 wa dhahabu nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kuanza mgomo kudai nyongeza ya mishahara.
Chama cha kitaifa cha wafanyakazi wa migodini kinataka waongezwe mishahara kwa asilimia sitini.
Wafanyakazi hao wiki jana walikataa pendekezo walilopewa la nyongeza ya asilimia 6 ambacho ni kiwango cha mfumuko wa bei kwa sasa.
Sekta ya madini ya dhahabu ndio moja ya sekta kubwa duniani lakini imekuwa ikikumbwa na misukosuko katika miaka ya hivi karibuni huku ile ya madini ya platinum ikijikwamua kutokana na athari za migomo iliyokumba sekta hiyo mwaka jana.
Inakisiwa kuwa migomo hiyo ya wachimbaji migodi ikiwa itafanyika, itapotezea nchi hiyo zaidi ya dola milioni 30 kila siku.
Wamiliki wa migodi wanaonya kuwa migomo hiyo huenda ikasababisha migodi ya dhahabu kufungwa na maelfu kupoteza kazi zao kufuatia kushuka kwa bei ya dhahabu.
Wanasema kuwa gharama za uchimbaji dhahabu zimepanda kwani wamelazimika kutumia pesa nyingi zaidi katika shughuli nzima za uzalishaji.
Kwa miezi mingi Afrika Kusini ilikuwa nchi yenye kuzalisha zaidi dhahabu ikiwa inazalisha asilimia 68 ya dhahabu yote duniani katika miaka ya sabini.
Lakini kwa sasa iko katika nafasi ya tano katika uzalishaji wa madini hayo ikiwa ni asilimia sita pekee ya dhahabu yote duniani ingawa bado ni sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi hiyo.
Rais Jocob Zuma ametaka pande zote mbili kwenye mgogoro huu kuafikiana ili kuzuia hasara kwa pande zote mbili.
Wafanyakazi watalazimika kuondoka kazini saa sita asubuhi kwa mujibu wa msemaji wa chama cha wafanyakazi hao, alisema Lesiba Seshoka.
Hata hivyo alikanusha madai kuwa nyongeza wanayotaka ya asilimia 60 ni kubwa sana. Chama cha wafanyakazi cha NUM kinawakilisha asilimia 64 ya wafanyakazi 120,000 wanaochimba dhabahu migodini.
Wananchi wa Afrika Kusini walishangazwa sana mwaka jana wakati polisi walipowaua wachimba migodi 34 wa Platinum waliokuwa wamefanya mgomo haramu uliokuwa umeitishwa na chama chao na kutuhumu NUM kuwa na uhusiano wa karibu na serikali.
Mwandishi wa BBC Mike Wooldridge mjini in Johannesburg anasema kuwa huku uchaguzi ukisubiriwa mwaka ujao,
serikali inatumai kuwa itaweza kukabili migomo hiyo, katika msimu huu ambapo watu wengi wanaomba nyongeza ya mishahara.

 Chanzo na BBC Swahili