Jumatano, 4 Septemba 2013

Muandaaji pambano la Cheka kutinga kortini


Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Suleiman Kova
Muandaaji wa pambano la kimataifa la ngumi kati ya bondia Francis Cheka wa Tanzania na Mmarekani Phil Williams, Jay Msangi yuko katika hatari ya kuburuzwa mahakamani wakati wowote kuanzia leo kutokana na tuhuma za kumdanganya Mmarekani huyo na kutomlipa fedha walizokubaliana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kwamba muandaaji huyo bado anashikiliwa na polisi na kwamba, ikibainika ni kweli amedanganya na kutolipa fedha hizo kama walizokubaliana atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani.

Akieleza zaidi, Kova alisema kuwa kwa kawaida huwa kuna mambo matatu yanayofanywa kabla ya pambano lote la ngumi na mojawapo ni makubaliano juu ya malipo.
 
"Mabondia kabla ya kupigana lazima wafanye mambo matatu... lazima waongee na mawakala wao, lazima wasaini mikataba kuhusiana na maslahi na pia wakubaliane kuwa watapigana kwa raundi ngapi," alisema Kova, akiongeza kuwa mwandaaji huyo bado anashikiliwa na polisi katika kituo cha Kati jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.

"Tunatakiwa kuwa wakali hata katika michezo kwavile mapambano ya aina hii yanayotajwa kuwa ni ya kimataifa huitangaza nchi hadi nje ya mipaka yetu... sisi (polisi) tunaendelea na uchunguzi wetu ili kubaini kilichotokea," alisema Kova.

Taarifa zaidi zilieleza baadaye jana kuwa muandaaji huyo anadaiwa na Mmarekani Williams dola za Marekani 8,200 (Sh. milioni 13).

Katika pambano hilo la raundi 12 kuwania mkanda wa WBF, uzani wa 'super middle' lililofanyika Ijumaa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Cheka alitwaa ubingwa huo baada ya kushinda kwa pointi.

Dalili za utata wa malipo katika pambano hilo zilianza kuonekana mapema baada ya mabondia Alfonce Mchumiatumbo aliyepigana na Chupac Chipindi katika pambano lao la utangulizi la raundi sita kugoma kupanda ulingoni hadi wamaliziwe pesa zao za mkataba wa kucheza mechi hizo kabla ya kupanda ulingoni, sawa na kile walichokifanya mabondia Mada Maugo na Thomas Mashali ambao pia walikataa kupanda ulingoni hadi walipohakikishiwa kulipwa fedha zao.

Hakuna maoni: