WAZIRI MKUU WA LIBYA ZAIDAN AACHIWA HURU
Picha ya Zeidan akitekwa nyara mjini Tripoli
Waziri mkuu wa Libya ameachiliwa saa chache baada ya
kutekwa nyara na watu wanaominika kuwa wapiganaji wa kiisilamu. Hii ni
kwa mujibu wa serikali ya Libya.
Ali Zeidan alitekwa nyara na kundi la waasi waliokuwa na uhusiano na serikali kwa jina Revolutionaries Operations Room.
Walisema walimteka nyara kwa maagizo ya mwendesha mkuu wa mashtka ingawa wizara ya sheria imekanusha madai hayo.
Kundi hilo lilikuwa miongoni mwa makundi ya
wapiganaji walioghadhabishwa na hatua ya makomandao wa Marekani
kumkamata Anas Al-Liby mshukiwa wa kundi la kigaidi la al-Qaeda .
Wengi walitaja hatua ya Marekani kama ya
kuingilia uhuru wa taifa hilo na kata kutaka maelezo kutoka kwa balozi
wa Marekani nchini humo.
Mwandishi wa BBC mjini humo anasema Zeidan alitekwa nyara akiwa ndani ya hoteli ya kifahari anamoishi.
Serikali imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kali
baada ya makomando wa Marekani kumkamata mmoja wa viongozi wa al-Qaeda
Anas al-Liby nchini Libya.
Bwana Liby alikamatwa Jumamosi mjini Tripoli kwa
madai ya kuhusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya
balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 2008.
Mnamo siku ya Jumatatu Libya ilimhoji balozi wa Marekani kuhusu kukamatwa Al Liby.
Kwa upande wake Zeidan alitoa wito kwa Marekani
na nchi za Magharibi kuisaidia serikali ya Libya kukomesha vitendo vya
wapiganaji wenye itikadi kali nchini humo.
Kwenye mahojiano na BBC, alisema kuwa Libya inatumiwa kama kambi ya kuweka silaha.
Waziri mkuu aliambia BBC kuwa nchi yake inatumia
kama kivukio cha kusafirishia silaha kwenda katika maeneo mengine ya
kanda hiyo.
TAYLOR KUHUDUMIA KIFUNGO UINGEREZA
Taylor akisikiliza kesi dhidi yake mjini Hague
Aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor atahudumia
kifungo chake cha miaka 50 jela nchini Uingereza baada ya kupatikana na
hatia ya uhalifu wa kivita.
Haya ameyasema waziri wa sheria nchini Uingereza Jeremy Wright.
Sweden na Rwanda pia zilikuwa zimeomba kumfunga
jela Taylor katika ardhi yao baada ya rufaa yake kukataliwa na mahakama
mwezi jana.
Taylor alihukumiwa kifungo cha miaka 50 jela na mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Sierra Leone, mjini Hague.
Iliamua kuwa makosa dhidi yake yalithibtishwa bila tashwishi.
Alihukumiwa jela mwaka 2012 kwa kuwasidia waasi
waliofanya maasi makubwa dhidi ya watu wa Sierra Leone wakati wa vita
vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Taylor, mwenye umri wa miaka 65, alipatikana na
hatia ya kuwapa waasi wa Revolutionary United Front silaha na wao
wakimpa almasi kutoka Sierra Leone.
MISRI YAKOSOA MAREKANI KWA KUBANA MSAADA
Marekani intaka Misri kuhakikisha uchaguzi huru na haki unafanyika kabla ya kuipa msaada tena
Serikali ya misiri imekosoa
Marekani kufuatia uamuzi wake wa kusitisha awamu nyingine ya msaad wa
kijeshi kwa serikali yake inayoungwa na jeshi la nchi hiyo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Misri
amesema, taifa hilo haliwezi kuhujumiwa na uamzui huo akisema kuwa
serikali ya Misri itaendelea na kile alichokitaja kama mkondo wake wa
kuafikia utawala wa demokrasia.
Marekani ilibana sehemu kubwa ya dola bilioni 1.3 ambazo hutolewa kwa Misri kama msaada wa kijeshi.
Kutolewa kwa zana za kijeshi pamoja na msaada wa
kifedha kwa serikali ya Misri itabanwa. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya
mambo ya nje ya Marekani.
Imesema kuwa hatua lazima zichukuliwe katika kuhakikisha kuna uchaguzi huru na wa haki kama kikwazo cha kupata msaada huo tena.
Hataua hii inatokana na Marekani kudurusu hali
nchini Misri baada ya maafisa wa utawala kumwondoa mamlakani Morsi na
kusababisha idadi kubwa ya vifo miongoni mwa wafuasi wake.
"Tutatendelea kuzuia msaada mkubwa wa kijeshi
kwa Misri hadi itakapochukua hatua za kuhakikisha kuna serikali halali
mamlakani na ambayo imechaguliwa kihalali na kwa njia ya kidemokrasia,’’
alisema msemaji wa idara ya mamambo ya ndani wa Marekani Jen Psaki.
Maafisa walisema kuwa kubanwa kwa msaada huo,
kutakosesha Misri kupata mamilioni ya dola pamoja na ndege aina ya
Apache helikopta, pamoja na makombora ya Harpoon na sehemu za vifaru vya
kijeshi.
Serikali pia inapanga kubana dola milioni 260 kwa serikali ya Misri pamoja na mkopo wa dola milioni 300.
Hata hivyo wadadisi wanasema kuwa hatua hii sio
kali sana kwa Misri na kuwa ilitarajiwa hasa kutoipa Misri zana za
kijeshi, na mafunzo ambayo pia hayatatolewa hadi masharti yatimizwe.
Aidha itaendelea kutoa msaada wa kiafya na elimu pamoja na kuakikisha kuwa usalama unadhibitiwa katika rasi ya Sinai.
CHANZO NA BBC SWAHILI