Jumatano, 16 Oktoba 2013

USIPITWE NA MATUKIO MBALIMBALI YANAYOTOKEA POPOTE ULIMWENGUNI

WATU WATATU WAZUILIWA KWA MAUAJI HUKO AFRIKA KUSINI
 
 
Mtaa wa Dieplsloot una watu wengi wanaoishi kwa umaskini

Watu watatu wamezuiliwa nchini Afrika Kusini kuhusiana na mauaji ya watoto wawili ambayo yalizua ghasia katika mtaa wa Diepsloot.
Kwa mujibu taarifa ya polisi, miili ya wasichana wawili walio na umri wa miaka miwili na mitatu ilipatikana imetpwa kwenye choo cha umma siku ya Jumanne baada ya wawili hao kupotea siku ya Jumamosi.
Ghasia zilizuka huku wenyeji wakiwatuhumu polisi kwa kukosa kulinda jamii ipasavyo.
Rais Jacob Zuma aliwasihi wasichukue sheria mikononi mwao.
"kitendo hiki cha unyama dhidi ya watoto wetu, sio kitu ambacho kinapaswa kufanywa katika jamii hii ambayo daima tunajitahidi kuiunda,'' alinukuliwa akisema Rais Zuma kwenye jarida moja la mtaani Soweto.
''Tunalaani vikali mauaji haya.''
Luteni kanali Lungelo Dlamini, alisema kuwa watu watatu wanahojiwa na polisi na kuwa wangali wanamsaka mtu wa nne anayeshuiwa kuhusika na kitendo hicho.
Alisema kuwa pia wanachunguza kuwepo uhusiano kati ya mauaji hayo na yale ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano aliyepatikana amefariki katika eneo hilo hilo, mwezi Septemba.
Kulingana na jarida la Star wenyeji wa Diepsloot, jamii masikini Kaskazini kwa Johannesburg, waliweka vizuizi barabarani na kuchoma magurudumu ya magari.
Maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni, yaliporwa huku waandishi wa habari wakishambuliwa.
Wasichana haio walikuwa na uhusiano wa kifamilia , na walipotea Jumamosi nyumbani kwao wakiwa wanacheza na marafiki zao.

MAELFU WATOROKA GHASIA HUKO AFRIKA YA KATI
 
Waasi wa Seleka wanasemekana kuzua rabsha upya katika maeneo ya Magharibi mwa nchi
Shirika la misaada la Medecins Sans Frontieres (MSF), limesema kuwa maelfu ya watu wamelazimika kutoroka makwao katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ghasia zilizoibuka upya.
Nchi hiyo yenye utajiri wa madini, imekuwa ikikumbwa na misukosuko, tangu waasi kumng'oa mamlakani Rais Francois Bozize mnamo mwezi Machi.
Serikali ya Ufaransa wiki hii ilisema kuwa itatuma wanajeshi wa ziada nchini humo katika juhudi zake za kumaliza mgogoro nchini humo.
Wafanyakazi wa afya kutoka katika shirika hilo, wanasema kuwa wanashuhudia visa vya mauaji nchini humo.
Wanawake na watoto ni miongoni mwa watu waliothirika zaidi na ambao wanatibiwa kwa majeraha ya risasi , panga na silaha zengine za kijadi magharibi mwa nchi.
Wafanyakazi wa mashirika ya misaada pia wamekuwa wakishambuliwa.
Vijiji vyote vimeteketezwa na shirika hilo limesema kuwa limepokea visa vya mashambulizi yanayotokana na migawanyiko ya kidini.
Mapigano kati ya makundi ya kutoa ulinzi kwa wanakijiji pamoja na waasi wa zamani yamewalazimisha maelfu kutoroka makwao huku shirika hilo likisema kuwa hali ya kibinadamu sasa ni ya kusikitisha sana na inahitaji kushughulikiwa kwa dharura.

44 WAFARIKI KWA AJALI YA NDEGE LAOS
Uwanja wa ndege Luang

Abiria wote waliokuwa wameabiri ndege nchini Laos wamefariki baada ya ndege iliyokuwa imewabeba kuanguka Kusini mwa nchi.
Maafisa katika nchi jirani ya Thailand wamesema kuwa ndege hiyo ilianguka ndani ya mto Mekong.
Aidha inaarifiwa kuwa ndege hiyo ilianguka kutokana na hali mbaya ya hewa muda mfupi kabla ya kutua katika uwanja wa Pakse.
Ndege hiyo ilikuwa inatoka katika mji mkuu wa Laos wa Vientiane ilipoanguka asubuhi ya leo.
Msemaji katika wizara ya mambo ya nje Sek Wannamethee alisema kuwa abiria 39 na wafanyakazi 4 walikuwa ndani ya ndege hiyo
Alisema rai watano wa Thailand walikuwa miongoni mwa waliofariki.