Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto anakwenda The Hague, Uholanzi, leo
ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kesi inayomkabili katika Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya
Binaadamu (ICC) mjini humo.
Ruto mwenye umri wa miaka 46 anakabiliwa na mashitaka ya kuandaa
machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo mamia ya watu
waliuwawa.
Kiongozi huyo ni mwanasiasa wa ngazi ya juu kabisa aliye madarakani
kuwahi kufika mbele ya mahakama hiyo ahadi sasa na kesi hiyo itaanza
siku chache tu baada ya wabunge nchini Kenya kupiga kura kujitoa katika
mahakama na kuwa nchi ya kwanza kuchukua hatua hiyo.
Wakati akiondojka kwenye uwanja wa ndege wa Nairobi, Makamu huyo wa rais
aliupungia mkono umati uliokuweko uwanjani, lakini alikataa kusema
chochote.
Ruto anatuhumiwa kupanga baadhi ya machafuko yaliozuka baada ya uchaguzi
2007-2008 ambapo watu wapatao 1,100 waliuwawa na zaidi ya 600,000
kupoteza makaazi yao.
Mshitakiwa mwenzake, mtangazaji wa kituo kimoja cha Redio Joshua arap
Sang anayetuhumiwa kuratibu mashambulizi hayo, tayari yuko The Hague,
ambako aliwasili mwishoni mwa juma. Wopte wamesema watakana mashtaka
yanayowakabili.
Jumapili Ruto alishiriki katika sala ya maombi kanisani akiwa pamoja na
Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia anatuhumiwa kuandaa kampeni ya mauaji,
ubakaji na kuwahamisha watu. Kesi dhidi yake itaanza Novemba 12
Kenyatta asema hatakwenda The Hague kama Ruto hajarejea
Hata hivyo Rais Kenyatta amesema hatokubali yeye na naibu wake wawe nje ya Kenya kwa wakati mmoja.
"Tutashirikiana na mahakama ya ICC na wakati wote tumekuwa tukiahidi
kufanya hivyo," aliuambia mkutano wa hadhara wa wafuasi wake kwamba
lazima ifahamike lakini kwamba Kenya ina katiba na kwamba Ruto na yeye
hawatokuwa nje ya nchi wakati mmoja.
Kenyatta ambaye pia atayakana mashtaka yanayomkabili amesema ni ya
uwongo na yatafutwa, akiongeza kwamba wapangaji wa njama hizo watatajwa
na kuaibishwa. Huku akishangiriwa na umati uliokuwa ukimsikiliza,
Kenyatta alisema,"shindi hautokuwa wa Ruto, Sanga au wangu , bali kwa
Kenya."
Uchaguzi wa 2007 nchini Kenya uliangamwa na madai ya wizi wa kura na
mizengwe, lakini kile kilichoanza ghasia za kisiasa kikageuka kuwa wimbi
la mauaji ya kikabila na mashambulizi ya kulipiziana kisasi, yakiwa
machafuko mabaya kabisa tangu huru wa nchi hiyo 1963
Mwaandsishi: Mohammed Abdul-Rahman/AFP
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kulia) na Makamu wake, William Ruto.
Mhariri: Josephat Charo