Alhamisi, 10 Oktoba 2013

YAJUE YANAYOENDELEA DUNIANI KUPITIA HAPA FREE MEDIA TO BLOGS

WAZIRI MKUU WA LIBYA ZAIDAN AACHIWA HURU


Picha ya Zeidan akitekwa nyara mjini Tripoli
Waziri mkuu wa Libya ameachiliwa saa chache baada ya kutekwa nyara na watu wanaominika kuwa wapiganaji wa kiisilamu. Hii ni kwa mujibu wa serikali ya Libya.
Ali Zeidan alitekwa nyara na kundi la waasi waliokuwa na uhusiano na serikali kwa jina Revolutionaries Operations Room.
Walisema walimteka nyara kwa maagizo ya mwendesha mkuu wa mashtka ingawa wizara ya sheria imekanusha madai hayo.
Kundi hilo lilikuwa miongoni mwa makundi ya wapiganaji walioghadhabishwa na hatua ya makomandao wa Marekani kumkamata Anas Al-Liby mshukiwa wa kundi la kigaidi la al-Qaeda .
Wengi walitaja hatua ya Marekani kama ya kuingilia uhuru wa taifa hilo na kata kutaka maelezo kutoka kwa balozi wa Marekani nchini humo.
Mwandishi wa BBC mjini humo anasema Zeidan alitekwa nyara akiwa ndani ya hoteli ya kifahari anamoishi.
Serikali imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kali baada ya makomando wa Marekani kumkamata mmoja wa viongozi wa al-Qaeda Anas al-Liby nchini Libya.
Bwana Liby alikamatwa Jumamosi mjini Tripoli kwa madai ya kuhusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 2008.
Mnamo siku ya Jumatatu Libya ilimhoji balozi wa Marekani kuhusu kukamatwa Al Liby.
Kwa upande wake Zeidan alitoa wito kwa Marekani na nchi za Magharibi kuisaidia serikali ya Libya kukomesha vitendo vya wapiganaji wenye itikadi kali nchini humo.
Kwenye mahojiano na BBC, alisema kuwa Libya inatumiwa kama kambi ya kuweka silaha.
Waziri mkuu aliambia BBC kuwa nchi yake inatumia kama kivukio cha kusafirishia silaha kwenda katika maeneo mengine ya kanda hiyo.

TAYLOR KUHUDUMIA KIFUNGO UINGEREZA
 
Taylor akisikiliza kesi dhidi yake mjini Hague
Aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor atahudumia kifungo chake cha miaka 50 jela nchini Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita.
Haya ameyasema waziri wa sheria nchini Uingereza Jeremy Wright.
Sweden na Rwanda pia zilikuwa zimeomba kumfunga jela Taylor katika ardhi yao baada ya rufaa yake kukataliwa na mahakama mwezi jana.
Taylor alihukumiwa kifungo cha miaka 50 jela na mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Sierra Leone, mjini Hague.
Iliamua kuwa makosa dhidi yake yalithibtishwa bila tashwishi.
Alihukumiwa jela mwaka 2012 kwa kuwasidia waasi waliofanya maasi makubwa dhidi ya watu wa Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Taylor, mwenye umri wa miaka 65, alipatikana na hatia ya kuwapa waasi wa Revolutionary United Front silaha na wao wakimpa almasi kutoka Sierra Leone.

MISRI YAKOSOA MAREKANI KWA KUBANA MSAADA
 
Marekani intaka Misri kuhakikisha uchaguzi huru na haki unafanyika kabla ya kuipa msaada tena
Serikali ya misiri imekosoa Marekani kufuatia uamuzi wake wa kusitisha awamu nyingine ya msaad wa kijeshi kwa serikali yake inayoungwa na jeshi la nchi hiyo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Misri amesema, taifa hilo haliwezi kuhujumiwa na uamzui huo akisema kuwa serikali ya Misri itaendelea na kile alichokitaja kama mkondo wake wa kuafikia utawala wa demokrasia.
Marekani ilibana sehemu kubwa ya dola bilioni 1.3 ambazo hutolewa kwa Misri kama msaada wa kijeshi.
Kutolewa kwa zana za kijeshi pamoja na msaada wa kifedha kwa serikali ya Misri itabanwa. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya mambo ya nje ya Marekani.
Imesema kuwa hatua lazima zichukuliwe katika kuhakikisha kuna uchaguzi huru na wa haki kama kikwazo cha kupata msaada huo tena.
Hataua hii inatokana na Marekani kudurusu hali nchini Misri baada ya maafisa wa utawala kumwondoa mamlakani Morsi na kusababisha idadi kubwa ya vifo miongoni mwa wafuasi wake.
"Tutatendelea kuzuia msaada mkubwa wa kijeshi kwa Misri hadi itakapochukua hatua za kuhakikisha kuna serikali halali mamlakani na ambayo imechaguliwa kihalali na kwa njia ya kidemokrasia,’’ alisema msemaji wa idara ya mamambo ya ndani wa Marekani Jen Psaki.
Maafisa walisema kuwa kubanwa kwa msaada huo, kutakosesha Misri kupata mamilioni ya dola pamoja na ndege aina ya Apache helikopta, pamoja na makombora ya Harpoon na sehemu za vifaru vya kijeshi.
Serikali pia inapanga kubana dola milioni 260 kwa serikali ya Misri pamoja na mkopo wa dola milioni 300.
Hata hivyo wadadisi wanasema kuwa hatua hii sio kali sana kwa Misri na kuwa ilitarajiwa hasa kutoipa Misri zana za kijeshi, na mafunzo ambayo pia hayatatolewa hadi masharti yatimizwe.
Aidha itaendelea kutoa msaada wa kiafya na elimu pamoja na kuakikisha kuwa usalama unadhibitiwa katika rasi ya Sinai.

CHANZO NA BBC SWAHILI



Hakuna maoni: