Alhamisi, 19 Septemba 2013

HABARI ZA HIVI PUNDE:Vikosi vyakabiliana na wapiganaji Misri




Majeshi ya Misri yameraukia kwenye mji wa Kerdasah kuondoa kile wanachosema ni makundi ya kigaidi
Vikosi vya usalama nchini Misri, vimekabiliana na wapiganaji wa kiisilamu baada kuingia katika mji ulioko viungani vya mji mkuu Cairo wa Kerdasah.
Duru zinasema kuwa wanajeshi hao waliingia mjini humo ambako polisi 11 waliuawa mwezi jana kukabiliana na kile walichokiita magaidi.
Mauaji hayo yalitokea wakati aliyekuwa rais Mohammed Morsi alipoondolewa mamlakani na jeshi.

Vyombo vya habari vya serikali vimesema kuwa magari ya kivita yalifika mjini Kerdasah kabla ya asubuhi ya leo.
Maafisa walisema kuwa lengo la vikosi hivyo kuwepo hapo ni kuondoa magaidi na kumaliza magenge ya wahalifu .
Taarifa zinasema kuwa polisi mmoja ameuawa. Vikosi hivyo inasemekana vilifanya msako katika nyumba za watu eneo hilo hasa kuwatafuta wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood.
Maafisa wa utawala waliahidi kuchukua hatua kufuatia mauaji ya polisi yaliyofanyika mwezi Agosti, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Inaarifiwa kuwa naibu waziri wa mambo ya ndani, alishauriana na wanajeshi hao kabla ya kuanza msako wao.
Baada ya sala ya asubuhi, wanajeshi hao walianza kuchukua nafasi zao kujiweka tayari kwa makabiliano.
Mji wa Kerdasah, unaosifika kwa kuzalisha na kuuza vitambaa vya nguo uko umbali wa kilomita 14 kutoka mjini Cairo.Wenyeji wa mji huo walinukuliwa wakisema kuwa hawana imani na polisi.

Hakuna maoni: