Jumatatu, 16 Septemba 2013

YANGA WAMEKATA RUFAA MECHI YAO DHIDI YA MBEYA CITY



Kabla ya mchezo huo kuanza kulitokea vurugu za mashabiki baada ya mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Mbeya City kulipiga mawe basi la Yanga wakati linaingia uwanjani pamoja na gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba viongozi wa Yanga nalo lilipigwa mawe na kioo cha nyuma cha gari kuvunjika.
Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamekata rufaa kwa kamati ya Ligi kutaka mchezo wao dhidi ya Mbeya City uliofanyika Jumamosi iliyopita urudiwe kwenye uwanja huru.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine ulimalizika kwa sare ya 1-1 na kufanikiwa kuingiza Sh100 milioni baada ya mashabiki 20,000 kushuhudia mechi hiyo.
Kabla ya mchezo huo kuanza kulitokea vurugu za mashabiki baada ya mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Mbeya City kulipiga mawe basi la Yanga wakati linaingia uwanjani pamoja na gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba viongozi wa Yanga nalo lilipigwa mawe na kioo cha nyuma cha gari kuvunjika.
Wakizungumza jijini Mbeya, Ofisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto akisaidiana na mjumbe wa kamati ya sekretarieti ya Yanga, Patrick Naggi walisema, “Tunachohitaji mechi irudiwe na ichezwe kwenye uwanja huru.”

“Tunataka mechi ichezwe kwenye uwanja huru kwa sababu ya matukio yaliyotokea katika mechi yetu dhidi ya Mbeya City ambayo yaliifanya timu kucheza bila amani kutokana na vurugu zilizokuwa zinafanywa na mashabiki wa Mbeya,” alisema Kizuguto.
“Basi la timu pamoja na Noah yaliyokuwa yamebeba wachezaji na viongozi yalishambuliwa na vioo kuvunjwa, pia dereva wa basi, Maulid Kihula na beki Nadir Haroub walijeruhiwa,” alisema Kizuguto na kusisitiza wanataka uangalizi zaidi mechi yao ijayo dhidi ya Prisons.
Naye Naggi alisema, “Tukio lile halikuwa la kimichezo, kila mtu aliyekuwa uwanjani aliona.”
Kutokana na madai hayo ya Yanga, msemaji wa Coastal Union, Edo Kumwembe ambao basi la wachezaji wao lilipigwa mawe na mashabiki wa Yanga jijini Dar es Salaam ametaka mechi yao pia irudiwe.
Wakati huohuo; Kocha mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema waliingia uwanjani kwa lengo la kuhakikisha washambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu na Jerry Tegete hawafurukuti.
“Unajua tulijiandaa kwa mambo mengi, kama unavyojua Yanga ni timu kubwa na ndiyo mabingwa watetezi kama tungefanya mchezo wangetudhalilisha,” alisema Mwambusi. Naye kocha wa Yanga, Ernest Brandts alisema wamepata matokeo hayo kutokana na sababu mbalimbali moja ni uwanja mbovu.
“Staili ya mchezo ni kubutuabutua tu kama Ragbi wakati Yanga tunapenda kucheza mpira,” alisema Brandts.

Hakuna maoni: