Alhamisi, 24 Oktoba 2013

JE,UMEISIKIA HII POPOTE PALE AU UNATAKA KUISIKIA HAPA?

Makinda: Wabunge waliotemwa wamepigika

Adai wanakwenda ofisini kwake kuombaomba
 
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amesema kuwa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili wabunge wanapomaliza vipindi vyao, ofisi yake imelazimika kutoa mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kumudu maisha.
Makinda alitoa kauli hiyo jana wakati akibadilishana mawazo na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf ambaye yupo nchini kwa mapumziko mafupi na familia yake.
Alisema kuwa kwa kipindi alichokaa katika kiti cha uspika, amebaini matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wabunge waliostaafu.
Makinda alisema kuwa wabunge wengi wamekuwa wakiathirika kiuchumi pindi wanapotoka katika nafasi hiyo, hivyo mafunzo yatawawezesha kuwa na shughuli za kufanya, na kwamba yatatolewa kwa wabunge wote.
Alisema kuwa ni muhimu wabunge wakaichukulia siasa kuwa sio kazi ya kudumu ili wanaposhindwa kuchaguliwa, wafanye shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.
“Hata ukiangalia magomvi yanayotokea wakati wa uchaguzi, wengi wasiokubali matokeo ni wale ambao hawana shughuli za kufanya,” alisema.
Spika Makinda alisema kuwa kwa wabunge ambao wana shughuli za kufanya, kwao ubunge unakuwa sio tatizo kwa kuwa wana uwezo wa kuendesha maisha yao.
Alisema tangu ashike nafasi hiyo, wabunge wengi walioshindwa uchaguzi wamekuwa wakifika ofisini kwake na kuomba msaada wa kifedha wakati ofisi hiyo haina fungu la wastaafu hao.
“Kuna siku nilikuwa ofisini walikuja wabunge wastaafu zaidi ya watano wakiomba msaada, ikanilazimu nitoe akiba yangu nikawasaidia baadhi, lakini wale ambao hawakupata chochote walinung’unika sana,” alisema.
Makinda alisema kuwa kabla ya mwaka 1995, Bunge liliweka utaratibu wa pensheni kwa wabunge wastaafu, lakini uliondolewa na anachopata sasa mbunge ni posho ya kumaliza vipindi vyake vya ubunge.
Alisema kuwa na hiyo inatokana na mishahara midogo wanayopata wabunge ukilinganisha na mabunge mengine.
“Hata ukiangalia fedha unayopata, unatakiwa kuigawa na nyingine kupeleka jimboni, nyingine wengine wanatumia wakati wa uchaguzi jambo linalofanya mbunge akikosa kuchaguliwa akose la kufanya,” alisema.
Naye Graf, alisema kuwa wabunge wa nchi yao hawana shida pale wanaposhindwa kuchaguliwa kwa kuwa wana uwezo wa kupata kazi nyingine, na ajira sio tatizo.

Hakuna maoni: