Ijumaa, 1 Novemba 2013

LIGI KUU TANZANIA BARA YAINGIA DOSARI NI BAADA YA MASHABIKI WA SIMBA KULETA VURUGU UWANJANI

 
Kikosi cha Klabu ya Simba ya Tanzania

Polisi jijini Dar es Salaam Tanzania wamelazimika kutumia Mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa Klabu ya Simba,baada ya kumalizika mechi ya Ligi kuu soka Tanzania bara siku ya Alhamis ambapo Simba ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na timu ya Kagera Sugar.
Vurugu hizo zimezuka mwishoni mwa mechi ambayo timu ya Simba imezidi kuporomoka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo kufuatia matokeo ya sare ya bao 1-1.
Baada ya Simba kuongoza bao 1 hadi dakika ya 90 Kagera Sugar waliposawazisha kwa Penati iliyotiwa kimiani na beki wa zamani wa Simba Salum Kanoni ambapo mashabiki wanaoaminika kuwa wa Simba walianza kung'oa viti uwanjani hali iliyosababisha askari polisi kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya mashabiki hao.
Simba ilianza kuliona lango la Kagera Sugar katika dakika ya 45 baada ya mshambuliaji raia wa Burundi Amis Tambwe kufunga bao la kwanza lililodumu hadi mapumziko.
Katika Kipindi cha pili Simba walianza kucheza kwa kujihami hali iliyosababishga Kagera kukaribia lango lao mara kwa mara na hatimaye wakafanikiwa kusawazisha katika dakika ya 90.
Kwa matokeo hayo Simba imeporomoka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 21,huku Azam, wakishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na pointi 23 sawa na Mbeya City lakini wakitofautiana kwa magoli ya kufunga.
Yanga ni ya tatu kwa kuwa na pointi 22.

Hakuna maoni: