
Wanafunzi Albino wakiwa wamepumzika nje ya eneo la shule.
Shinyanga. Shule ya Msingi Maalumu Buhangija iliyopo Manispaa ya Shinyanga ililenga kuwasaidia watoto wasioona.
Lakini kutokana na kuzuka kwa wimbi la mauaji ya
walemavu wa ngozi (albino), mwaka 2009 shule hiyo iliamua kuwahifadhi
hapo ili kulinda usalama wao pamoja na kuwapatia elimu.
Shule hiyo kwa sasa inalea watoto mchanganyiko
wakiwemo wasiiona 37, viziwi 46 na walemavu wa ngozi (albino) 164,
ambapo licha ya kuwa chini ya Serikali kupitia halmashauri husika, kwa
kiasi kikubwa inategemea msaada kutoka kwa wafadhili ambao ni mashirika,
wahisani pamoja na watu binafsi kutokana na Serikali kuitelekeza.
Watoto wanaosoma Buhangija Maalumu, wamekuwa
wakiishi kwa dhiki kubwa kutokana na uhaba wa fedha za kuwahudumia,
mahitaji muhimu kama vile chakula, malazi
na matibabu hali ambayo huwafanya kushinda njaa au kupata mlo mmoja kwa siku au pengine kushindia uji.
na matibabu hali ambayo huwafanya kushinda njaa au kupata mlo mmoja kwa siku au pengine kushindia uji.
Katika mahojiano na gazeti hili, mwalimu mkuu wa
shule hiyo Peter Ajali, anasema kuwa watoto hao wapo chini ya Serikali
kupitia halmashauri husika iliyoelekezwa kuwa kila mtoto alipiwe Sh2,500
kwa siku, ikiwa ni gharama ya chakula, matibabu pamoja na makazi bora,
lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na mzigo huo
kuegemea Manispaa ya Shinyanga pekee.
Mwalimu huyo anasema kuwa halmshauri zote za Mikoa
ya Shinyanga, Simiyu pamoja na Geita ambazo zina watoto shuleni hapo
zilitakiwa kutoa kiasi hicho cha fedha, lakini zimekuwa hazifanyi hivyo
jambo linalosababisha kuwa na deni la zaidi ya Sh180 milioni hadi sasa.
“Hapa shuleni kuna walemavu wa ngozi kutoka wilaya
za Mikoa ya Shinyanga, Simiyu pamoja Geita, hivyo kila wilaya
inawajibika kwa watoto wake kwa kuwalipia Sh2,500 kwa siku, lakini cha
kusikitisha ni kuwa mzigo huo umeachiwa Halmashauri ya Manispaa hii
(Shinyanga) na ndiyo sababu matatizo haya hayatatuliki,” anasema Mwalimu
Ajali.
Anatolea mfano kuwa mwezi Machi mwaka huu,
Serikali ilituma Sh19 milioni ikiwa ni bajeti ya miezi mine, ambayo ni
sawa na Sh6 milioni kwa kila mwezi, huku bajeti ya chakula pekee shuleni
hapo kwa mwezi ikiwa ni zaidi ya Sh13, tofauti na gharama nyingine kama
vile maji, umeme na matibabu .
Kuhusu wazazi wao
“Kwa kweli uendeshaji wa shule hii ni kazi ngumu,
kwani wakati mwingine tunalazimika kukopa madukani ili watoto hawa
wasilale njaa, kwani kula mlo mmoja au kushindia uji ni jambo la kawaida
shuleni hapa,” anaeleza Mwalimu Ajali.
Akizungumzia upande wa walemavu wa ngozi mwalimu
huyo anasema kuwa wengi wanafunzi hao wametelekezwa na wazazi wao kwani
tangu walipofikishwa kituoni hapo, wazazi hawajawahi kurudi kufuatilia
maendeleo ya watoto wao kielimu wala kiafya, jambo ambalo linaongeza
mzigo kwa shule hiyo kutokana na kukosa ushirikiano kutoka kwa wazazi
husika.
“Iwapo wazazi wangekuwa wanakuja mara kwa mara,
huenda hili tatizo lingepungua kwani nina imani wangewasaidia mambo
machache kama mavazi na matibabu. Lakini ni asilimia 6 hadi 25 pekee
hufika shuleni hapo kwa mwaka, tena mara moja kuwaangalia watoto wao,
huku asilimia 75 wakiwa hawafiki kabisa,”analalamika Ajali.
Kutokana na hali hiyo mwalimu mkuu huyo anasema kuwa hajui
hatima ya watoto hao watakapomaliza shule kwani hata wakati wa likizo
huwa hawaendi nyumbani kwa kuhofia usalama wao, huku wengine wakiwa
hawafahamu makwao kutokana na kuletwa shuleni hapo wakiwa na umri mdogo
wa miaka mitano huku wazazi wao wakiwatelekeza moja kwa moja.
Ajali anasema kuwa, pia shule hiyo inakabiliwa na
uhaba wa mabweni kwa wasichana na wavulana akieleza kwamba mabweni
yaliyopo yana uwezo wa kukaa watoto 100, lakini kwa sasa yana watoto
247.
Anaeleza kuwa kutokana na changamoto hiyo, watoto
hao wanalazimika kulala wanne katika kitanda kimoja, badala ya watoto
wawili, ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 147.
Hata hivyo, anasema kuwa Serikali pia imeshindwa
kuwahudumia walemavu hao kwa kuwapatia mafuta maalumu ya kuwakinga na
mionzi ya jua, jambo ambalo linawaleka katika mazingira na wakati mgumu
kwani ngozi zao zinaathiriwa zaidi na mionzi ya jua.
Akizungumzia elimu Mwalimu Ajali alisema kuwa,
kitaaluma watoto hao wanaonyesha jitihada kubwa huku wengi wao
wakisomeshwa kwa ufadhili wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS) la
nchini Canada, ambalo hadi sasa linasomesha watoto 51 elimu ya msingi na
sekondari, ambapo lengo kuwasomesha hadi chuo kikuu.
Kwa upande mwingine anasema kuwa kituo hicho
kinakabiliwa na uhaba wa walezi na kwamba waliopo hawakidhi mahitaji,
huku walezi wakiwa 12 na wanane kati yao, wameajiriwa na UTSS, wanne
wameajiriwa na Serikali, huku mahitaji halisi ni kuwa na walezi 20.
Asemavyo DC
“Pia kuna tatizo la madai ya wapishi na walinzi
kwani wana muda mrefu, zaidi ya miezi saba hawajalipwa mishahara yao.
Kwa kweli inasikitisha kuona mtu anafanya kazi muda wote huo lakini
halipwi, kwa upande mwingine naweza kusema wana moyo wa pekee kwani bado
wanafanya kazi kwa moyo mmoja,” anasema.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Annarose
Nyamubi akiwa shuleni hapo hivi karibuni anawataka wazazi na walezi wa
watoto hao kujenga tabia ya kuwatembelea mara kwa mara ikiwa ni pamoja
na kuwachukua wakati wa likizo ili kuwa karibu na familia zao.
Nyamubi aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa
kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo iliyoeleza kwamba wengi wa wazazi
na walezi wamewatelekeza watoto wao, huhu mkuu huyo wa wilaya
akisisitiza kuwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao akiwahakikishia
ulinzi na usalama wao wawapo nyumbani wakati wa likizo.
Wanafunzi wanasemaje?
Kwa upande wao wanafunzi hao (walemavu wa ngozi)
wanasema kuwa licha kukumbana na changamoto nyingi shuleni hapo zikiwemo
uhaba wa chakula, mabweni, matibabu, mafuta maalumu ya kujikinga ya
mionzi ya jua pamoja na vifaa vya kujifunzia, wamekuwa wakiendelea
kuishi shuleni hapo hata baada ya likizo kwa kuhofia usalama wao wawapo
nyumbani kwao.
Semeni Deus (13) mwanafunzi wa darasa la sita anasema kuwa
alitokea Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu mwaka 2010 kutokana na
kushamiri kwa mauaji ya albino na kwamba amekuwa akiishi shuleni hapo
siku zote hata wakati wa likizo huku wazazi wake wakija kumsalimia.
“Mimi nimetoka Wilaya ya Kahama tangu mwaka 2009,
lakini tangu nimekuja hapa sijawahi kurudi nyumbani kutokana na kuhofia
usalama wangu. Ila tuna shida sana hapa shuleni kama vile chakula kwani
hakitoshi hali inayosababisha wakati wa kula kunyang’anyana. Pia kuna
tatizo la malazi, bwenini tumebanana sana, matibabu pamoja na mavazi na
mafuta ya kujikinga na mionzi ya jua, ” anasema Hassan Khamis mwanafunzi
wa kidato cha pili.
Wanaiomba Serikali iwasaidie wakieleza kuwa
wanaishi kwa dhiki kubwa na kwamba hawana pa kukimbilia zaidi ya
kuitegemea Serikali ambayo imewasaidia kulinda usalama wao hadi sasa
shuleni hapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni