Ijumaa, 13 Septemba 2013

UNHCR - Tanzania haijawafukuza wakimbizi


wahamiaji haramu wahamishwa TZ sio wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, ofisi ya Tanzania limekanusha taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba, Tanzania imewarejesha nyumbani kwa nguvu, wakimbizi 25,000 wa Burundi mwezi mmoja uliopita.


Vilevile serikali ya Tanzania imesema, taarifa hiyo ni ya uzushi ambayo haina ukweli wowote na yenye nia ya kuichafulia jina nchi ya Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa kimbilio na makazi ya wakimbizi wengi kutoka nchi mbalimbali hasa za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Akizungumza na BBC, Mwakilishi Mkazi wa UNHCR nchini Tanzania , Bi. Joyce Mends Cole, amesema, amewasiliana na mwakilishi wa shirika hilo nchini Burundi ambaye amethibitisha kwamba hakuna wakimbizi wa nchi hiyo waliorejeshwa kutoka Tanzania.

Bi. Joyce amebainisha kuwa, tatizo lililopo ni kuchanganywa kwa maneno "Wakimbizi" na "Wahamiaji Haramu".

Amefafanua kwamba, katika operesheni inayoendelea kwa sasa nchini Tanzania, ya kuwasaka wahamiaji haramu huenda baadhi ya wakimbizi waliosalia wamekamatwa kimakosa.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Dk. Emmanuel Nchimbi, alimuhakikishia kuwa operesheni hiyo inafanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa ya haki za uhamiaji.

Katika hatua nyingine, serikali ya Tanzania kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Bw. Isaack Nantanga, imesema hakuna mkimbizi yeyote aliyerejeshwa Burundi kwa hiari wala kwa nguvu katika kipindi kilichotajwa.
Bw. Nantanga amebainisha kuwa, wakimbizi wote 264,000 ambao Tanzania imewapatia "Hifadhi ya Ukimbizi" wapo na wanaendelea kuishi kwenye kambi na makazi ya wakimbizi yaliyopo katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na Tanga.
Wakimbizi hao wanatoka katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, na Somalia.

Hadi Septemba nne mwaka huu, zaidi ya "Wahamiaji Haramu" 27,000 wamerejeshwa makwao kwa hiari ambao walikuwa wakiishi nchini Tanzania kinyume cha sheria katika mikoa ya Rukwa, Kigoma na Kagera

Hakuna maoni: